3 Daudi akatuma mtu kuuliza mwanamke huyo ni nani. Mtu huyo akamwambia Daudi “Mwanamke huyo ni Bathsheba binti wa Eliabu, na ni mke wa Uria Mhiti.”
4 Basi, Daudi alituma wajumbe wamlete. Basi Bathsheba akaja kwa Daudi, naye Daudi akalala naye; (mwanamke huyo alikuwa ndio tu amejitakasa baada ya hedhi yake); kisha akarudi nyumbani kwake.
5 Mwanamke huyo akapata mimba, naye akatuma habari kwa Daudi kuwa ana mimba yake.
6 Basi, Daudi akamtumia Yoabu ujumbe, “Mtume Uria, Mhiti kwangu.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi.
7 Uria alipofika kwake, Daudi alimwuliza habari za Yoabu, watu wote, na hali ya vita.
8 Halafu Daudi alimwambia Uria, “Rudi nyumbani kwako ukanawe miguu yako.” Uria alitoka nyumbani kwa mfalme, na mara mfalme akampelekea zawadi.
9 Lakini Uria hakurudi nyumbani kwake, bali alilala pamoja na watumishi wote wa bwana wake kwenye lango la ikulu.