Isaya 17 BHN

Mungu ataadhibu Ashuru na Israeli

1 Kauli ya Mungu dhidi ya Damasko.“Damasko utakoma kuwa mji;utakuwa rundo la magofu.

2 Mitaa yake imeachwa mahame milele.Itakuwa makao ya makundi ya wanyama,wala hakuna mtu atakayewatisha.

3 Ngome za kujihami za Efraimu zitatoweka,na utawala wa Damasko utakwisha.Waashuru ambao watabaki hai,watakuwa na fedheha kama wazawa wa Israeli.Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimenena.

Watakaosalia katika Israeli

4 “Siku hiyo, fahari ya Yakobo itaporomoshwa,na unono wake ataupoteza.

5 Atakwisha kama shamba lililovunwa,atafanyiwa kama mvunaji avunavyo nafaka,atakuwa kama shamba lililovunwa bondeni Refaimu.

6 Atabakiziwa wachache kama vile baada ya zeituni:Zeituni mbili, tatu katika tawi la juu;nne, tano katika matawi ya mti uzaao sana.Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nimenena.”

Mwisho wa kuabudu sanamu

7 Siku hiyo, watu watamwangalia Muumba wao, na kuelekeza macho yao kwa huyo Mtakatifu wa Israeli.

8 Hawatazielekea tena madhabahu ambazo ni kazi za mikono yao wenyewe, wala kuzitazamia tena kazi za mikono yao wenyewe, yaani sanamu za mungu Ashera na madhabahu za kufukizia ubani.

9 Siku hiyo miji yao imara itaachwa mahame, kama miji ambayo Wahivi na Waamori waliihama walipokuwa wakiwakimbia wazawa wa Israeli. Kila kitu kitakuwa uharibifu.

10 Maana wewe Israeli umemsahau Mungu aliyekuokoa,hukumkumbuka Mwamba wa usalama wako.Kwa hiyo, hata mkipanda mimea ya Baali,na kuiweka wakfu kwa mungu wa kigeni;

11 hata mkiifanya ikue siku hiyohiyo mliyoipandana kuifanya ichanue asubuhi hiyohiyo,mavuno yenu yatatowekasiku hiyo ya balaa na maumivu yasiyoponyeka.

Mataifa adui yanashindwa

12 Lo! Ngurumo ya watu wengi!Wananguruma kama bahari.Lo! Mlio wa watu wa mataifa!Yanatoa mlio kama wa maji mengi.

13 Mataifa yananguruma kama ngurumo ya maji mengi,lakini Mungu atayakemea, nayo yatakimbilia mbali.Yatafukuzwa kama makapi mlimani mbele ya upepo;kama vumbi litimuliwalo na kimbunga.

14 Wakati wa jioni yanaleta hofu kuu,lakini kabla ya asubuhi yametoweka!Hilo ndilo litakalowapata wanaonyakua mali yetu,ndilo litakalowapata wanaotupora.