1 “Nyinyi ni watoto wa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; msijichanje wala kunyoa upara kwa ajili ya mtu aliyefariki.
2 Nyinyi ni watu watakatifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; Mwenyezi-Mungu amewachagua muwe watu wake hasa, kati ya watu wote waishio duniani.
3 “Msile kitu kilicho chukizo kwa Mungu.
4 Mnaweza kula wanyama wafuatao: Ng'ombe, kondoo, mbuzi,
5 kulungu, paa, kongoni, mbuzimwitu, paa mweupe, pofu na mbuzi wa mlimani;
6 na kila mnyama mwenye kwato zilizogawanyika sehemu mbili na mwenye kucheua, huyo mnaweza kula.
7 Lakini msile mnyama yeyote ambaye kwato zake hazikugawanyika sehemu mbili na hacheui; msile ngamia, sungura na pelele, ingawa hucheua lakini kwato zao hazikugawanyika sehemu mbili; hao ni najisi kwenu.
8 Pia msile nguruwe, maana ijapokuwa kwato zake zimegawanyika sehemu mbili, yeye hacheui; hao ni najisi kwenu, msile nyama zao wala msiguse mizoga yao.
9 “Mnaweza kula kila aina ya samaki wenye mapezi na magamba.
10 Lakini kiumbe chochote kinachoishi majini kisicho na mapezi wala magamba msile; hivyo ni najisi kwenu.
11 “Mnaweza kula ndege wote walio safi.
12 Lakini msile ndege wafuatao: Furukombe, kipungu,
13 kengewa, kozi, mwewe kwa aina zake,
14 kunguru kwa aina zake,
15 mbuni, kirukanjia, dudumizi, kipanga kwa aina zake,
16 bundi, mumbi, bundi mkubwa,
17 mwari, nderi, mnandi,
18 membe, koikoi kwa aina zake, hudihudi na popo.
19 Na wadudu wote wenye mabawa ni najisi kwenu; msiwale.
20 Mnaweza kula viumbe vyote vyenye mabawa vilivyo safi.
21 Msile nyamafu yoyote; mnaweza kumpa mgeni anayeishi katika miji yenu, ale, au mnaweza kumwuzia mtu wa taifa lingine, kwa sababu nyinyi ni watakatifu na Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu. Msimchemshe mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.
22 “Toeni sehemu moja ya kumi ya mazao yenu yote ya shambani kila mwaka.
23 Halafu nendeni mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amepachagua kuweka jina lake, na mkiwa mbele yake mtaila zaka ya nafaka yenu, ya divai yenu na ya mafuta, na ya wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe na kondoo wenu; fanyeni hivi ili mjifunze kumcha Mwenyezi-Mungu Mungu wenu daima.
24 Ikiwa safari ni ndefu kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amechagua mahali pa kuweka jina lake ambapo ni mbali mno na nyumbani, nanyi hamwezi kubeba zaka za mazao yenu ambayo Mwenyezi-Mungu amewajalia kupata, basi, fanyeni hivi:
25 “Uzeni mazao yenu na kuchukua fedha hiyo mpaka mahali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alipopachagua,
26 mzitumie hizo fedha kwa chochote kile mtakachopenda – nyama ya ng'ombe, nyama ya kondoo, divai au kinywaji kikali; mtavila na kufurahi hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, pamoja na jamaa zenu.
27 Msiwasahau Walawi wanaoishi miongoni mwenu; wao hawana fungu wala urithi wao kati yenu.
28 Na kila mwisho wa mwaka wa tatu toeni zaka ya mazao yenu yote na kuyaweka akiba katika miji yenu.
29 Hiyo itakuwa kwa ajili ya Walawi, kwa kuwa hawana fungu wala urithi wao kati yenu, nao wageni, yatima na wajane ambao wanaishi katika miji yenu, watakuja kula na kushiba. Fanyeni hivi naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, awabariki katika kazi zenu zote mfanyazo kwa mikono yenu.