Waamuzi 2 BHN

Mwenyezi-Mungu anawagombeza watu wake

1 Malaika wa Mwenyezi-Mungu aliondoka Gilgali, akaenda Bokimu, akawaambia Waisraeli, “Niliwatoa nchini Misri na kuwaleta katika nchi ambayo niliwaahidi kwa kiapo babu zenu. Nilisema kwamba sitalivunja agano langu nanyi kamwe.

2 Na kwa upande wenu niliwaamuru msifanye agano na wenyeji wa nchi hii na kwamba madhabahu zao mtazibomoa. Lakini nyinyi hamkuitii amri yangu. Kwa nini mambo haya?

3 Kwa hiyo sasa nasema: Sitawafukuza tena wakazi wa nchi hii bali watawataabisha, nayo miungu yao itakuwa mtego kwenu.”

4 Malaika wa Mwenyezi-Mungu alipowaambia watu wote wa Israeli maneno haya, walipaza sauti zao na kulia.

5 Wakapaita mahali hapo Bokimu. Hapo wakamtolea sadaka Mwenyezi-Mungu.

Kifo cha Yoshua

6 Baada ya Yoshua kuwaaga Waisraeli, kila mmoja alikwenda kwenye eneo lake alilogawiwa ili kuimiliki nchi.

7 Waisraeli walimtumikia Mwenyezi-Mungu siku zote za maisha ya Yoshua na baada ya kifo chake muda wote walioishi wale wazee waliosalia ambao waliyaona matendo makuu ambayo Mwenyezi-Mungu aliwatendea Waisraeli.

8 Yoshua mwana wa Nuni na mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alifariki akiwa na umri wa miaka 110.

9 Wakamzika katika sehemu aliyogawiwa iwe yake huko Timnath-heresi, katika nchi ya milima ya Efraimu kaskazini ya mlima Gaashi.

10 Kisha watu wote wa kizazi chake walifariki, kikafuata kizazi kingine ambacho hakikumjua Mwenyezi-Mungu wala matendo aliyowatendea watu wa Israeli.

Waisraeli wanamwasi Mwenyezi-Mungu

11 Basi, Waisraeli walitenda uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuabudu Mabaali.

12 Walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wao, ambaye aliwatoa katika nchi ya Misri, wakaifuata miungu mingine, miungu iliyoabudiwa na watu walioishi kandokando yao. Waliisujudia miungu hiyo, wakamkasirisha sana Mwenyezi-Mungu.

13 Walimwacha Mwenyezi-Mungu, wakatumikia Mabaali na Maashtarothi.

14 Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka dhidi ya Israeli, naye akawaacha wanyanganyi wapore mali zao. Aliwakabidhi kwa adui zao waliowazunguka hata wasiweze tena kuwapinga.

15 Kila walipokwenda kupigana, mkono wa Mwenyezi-Mungu uliwakabili kuwaletea balaa, kama alivyokuwa amewaonya na kuapa. Nao wakawa katika huzuni kubwa.

16 Ndipo Mwenyezi-Mungu akawapa waamuzi ambao waliwaokoa mikononi mwa watu waliopora mali zao.

17 Hata hivyo, Waisraeli hawakuwasikiliza waamuzi wao, maana walifanya kama wazinzi kwa kufuata miungu mingine na kuisujudia. Waliacha upesi nyayo walizofuata babu zao ambao walitii amri za Mwenyezi-Mungu; bali wao hawakufanya hivyo.

18 Kila mara Mwenyezi-Mungu alipowapelekea mwamuzi, yeye mwenyewe alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa mikononi mwa adui zao muda wote wa uhai wa mwamuzi huyo. Aghalabu, Mwenyezi-Mungu aliwaonea huruma aliposikia kilio chao kutokana na mateso na dhuluma walizofanyiwa.

19 Lakini kila mara mwamuzi alipofariki walirudia mienendo yao ya zamani, wakaishi vibaya kuliko babu zao. Waliifuata miungu mingine, wakaitumikia na kuisujudia, wala hawakuyaacha matendo yao wala ukaidi wao.

20 Kwa hiyo Mwenyezi-Mungu akawaka hasira dhidi ya Waisraeli, akasema, “Kwa kuwa watu hawa wamevunja agano nililofanya na babu zao, wakakataa kutii sauti yangu,

21 sitayafukuza tena mataifa ambayo Yoshua aliyabakiza, wakati alipofariki.

22 Nitayatumia mataifa hayo kuwajaribu Waisraeli nione kama watairudia njia yangu kama babu zao au sivyo.”

23 Basi, Mwenyezi-Mungu akayaacha mataifa hayo, wala hakuyafukuza mara moja, wala hakumpa Yoshua ushindi juu ya mataifa hayo!

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21