Waamuzi 5 BHN

Wimbo wa Debora

1 Siku hiyo, Debora na Baraki, mwana wa Abinoamu, wakaimba wimbo huu:

2 “Viongozi walijitokeza kuongoza Israeli,watu walijitolea kwa hiari yao.Mshukuruni Mwenyezi-Mungu!

3 “Sikilizeni, enyi wafalme!Tegeni sikio, enyi wakuu!Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

4 “Ee Mwenyezi-Mungu, ulipotoka huko Seiri,ulipoteremka mlimani Edomu,nchi ilitetemeka,mbingu zilidondosha maji,naam, mawingu yakaiangusha mvua.

5 Milima ilitikisika mbele yako Mwenyezi-Mungu,naam, mlima Sinai mbele yako Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli.

6 “Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi,katika wakati wa Yaeli,misafara ilikoma kupita nchini,wasafiri walipitia vichochoroni.

7 Wakulima walikoma kuwako,walikoma kuwako katika Israeli,mpaka nilipotokea mimi Debora,mimi niliye kama mama wa Israeli.

8 Walijichagulia miungu mipya,kukawa na vita katika nchi.Lakini hakukupatikana mwenye upanga au ngaokati ya watu 40,000 wa Israeli.

9 Nawapa heshima makamanda wa Israeliwaliojitoa kwa hiari yao kati ya watu.Mshukuruni Mwenyezi-Mungu!

10 “Tangazeni, enyi wapandapunda weupe,enyi mnaokalia mazulia ya fahari,nyinyi mnaotembea njiani, tangazeni jambo hilo.

11 Imbeni kupita wanamuziki kwenye visima vya maji,tangazeni ushindi wa Mwenyezi-Mungu,ushindi kwa wakulima wake katika Israeli.Ndipo watu wa Mwenyezi-Mungu waliposhuka malangoni.

12 “Amka, amka, Debora!Amka! Amka uimbe wimbo!Amka, Baraki mwana wa Abinoamu,uwachukue mateka wako.

13 Mashujaa waliobaki waliteremka,watu wa Mwenyezi-Mungu walikwenda kumpiganiadhidi ya wenye nguvu.

14 Kutoka Efraimu waliteremka bondeni,wakafuata ndugu zao watu wa Benyamini;kutoka Makiri walishuka makamanda,kutoka Zebuluni maofisa wakuu.

15 Wakuu wa Isakari wakafuatana na Debora,watu wa Isakari waaminifu kwa Baraki;wakamfuata mbio mpaka bondeni.Lakini miongoni mwa koo za Reubenikulikuwamo kusitasita kwingi.

16 Kwa nini walibaki mazizini?Ili kusikiliza milio ya kondoo?Miongoni mwa koo za Reubenikulikuwamo kusitasita kwingi.

17 Kabila la Gileadi lilibaki ngambo ya Yordani.Kabila la Dani, kwa nini mlibaki merikebuni?Kabila la Asheri lilitulia huko pwani ya bahari,lilikaa bandarini mwake.

18 Watu wa Zebuluni ni watuwaliohatarisha maisha yao katika kifo.Hata wa Naftali walikikabili kifokwenye miinuko ya mashamba.

19 “Huko Taanaki, kando ya chemchemi za Megido,wafalme walikuja, wakapigana;wafalme wa Kanaani walipigana,lakini hawakupata nyara za fedha.

20 Nyota kutoka mbinguni zilishiriki vita,zilifuata njia zao, zilipigana na Sisera.

21 Mafuriko ya mto Kishoni yaliwachukua mbali,naam, mafuriko makali ya mto Kishoni.Songa mbele kwa nguvu, ee nafsi yangu!

22 “Farasi walipita wakipiga shoti;,walikwenda shoti na kishindo cha kwato zao.

23 Malaika wa Mwenyezi-Mungu asema hivi:‘Uapizeni mji wa Merosi,waapizeni vikali wakazi wake;maana hawakuja kumsaidia Mwenyezi-Munguhawakumsaidia Mwenyezi-Mungu dhidi ya wenye nguvu’.

24 “Abarikiwe kuliko wanawake woteYaeli, mke wa Heberi, Mkeni.Naam, amebarikiwa kuliko wanawake wotewanaokaa mahemani.

25 Sisera alimwomba maji, naye akampa maziwa;alimletea siagi katika bakuli ya heshima.

26 Kwa mkono mmoja alishika kigingi cha hema,na kwa mkono wake wa kulia nyundo ya fundi;alimponda Sisera kichwa,alivunja na kupasuapasua paji lake.

27 Sisera aliinama, akaanguka;alilala kimya miguuni pake.Hapo alipoinama ndipo alipoanguka, amekufa!

28 “Mama yake Sisera alitazama dirishanialichungulia katika viunzi vyake, akalalamika:‘Kwa nini gari lake limechelewa?Mbona vishindo vya magari yake vimechelewa kusikika?’

29 Jibu akalipata kwa wanawake wenye hekima:Akajituliza tena na tena kwa jibu hilo:

30 ‘Bila shaka wanatafuta na kugawana nyara;msichana mmoja au wawili kwa kila askari,vazi la sufu ya rangi kwa ajili ya Sisera.Vazi la sufu iliyotariziwa,na mikufu miwili ya nakshi kwa ajili ya shingo yangu!’

31 “Ee Mwenyezi-Mungu, waangamie adui zako wote!Lakini rafiki zako na wawe kama jua,wakati linapochomoza kwa mwanga mkubwa!”Nayo nchi ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21