1 Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni,
2 “Iwapo mtu yeyote atakuwa na uvimbe au upele au kipaku mwilini mwake, ikadhihirika kwamba ni ukoma, basi, ataletwa kwa kuhani Aroni au mmoja wa wanawe aliye kuhani.
3 Kuhani atapakagua mahali palipo na ugonjwa na ikiwa nywele za mahali hapo zimebadilika kuwa nyeupe na ugonjwa wenyewe ukionekana kuwa uko ndani zaidi ya ngozi ya mwili wake, basi, huo ni ukoma. Kuhani akimaliza kumkagua, hivyo atatangaza kuwa mtu huyo ni najisi.
4 Lakini ikiwa kipele hicho, ingawa cheupe hakikuingia ndani sana ya ngozi na wala nywele za mahali hapo hazikubadilika kuwa nyeupe, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda wa siku saba.
5 Siku ya saba, kuhani atamwangalia tena mtu huyo, na ikiwa, kulingana na uchunguzi wa kuhani, ugonjwa huo haujaenea kwenye ngozi yake, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku nyingine saba.
6 “Kuhani atamkagua tena mtu huyo siku ya saba. Kama kulingana na uchunguzi wake, ile sehemu ya ugonjwa imefifia na ugonjwa haujaenea, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi; huo ni upele tu. Mtu huyo atafua mavazi yake, naye atakuwa safi.
7 Lakini upele huo ukiwa umeenea kwenye ngozi, baada ya mtu huyo kujionesha kwa kuhani kwa ajili ya kutakaswa kwake, basi, atakuja tena kwa kuhani.
8 Kuhani atamwangalia tena, na kama ule upele umeenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; huo ni ukoma.
9 “Kama mtu ameshikwa na ukoma, ataletwa kwa kuhani.
10 Kuhani atamwangalia na kama kuna uvimbe mweupe ambao umezifanya nywele zake ziwe nyeupe na uvimbe huo umegeuka kuwa kidonda kibichi,
11 huo ni ukoma wa muda mrefu. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Hakuna haja ya kumweka mtu huyo kwa uchunguzi kwani yu najisi tayari.
12 Kama ukoma umemshika na umeenea mwili mzima, toka utosini hadi nyayoni kama atakavyoona kuhani,
13 hapo kuhani atamwangalia. Kuhani akiona kuwa ukoma umemwenea mwili mzima, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi kwa sababu mwili umegeuka kuwa mweupe na hivyo mtu huyo yu safi.
14 Lakini kukionekana mwilini mwa mtu huyo kidonda kibichi, basi, mtu huyo atakuwa najisi.
15 Kuhani ataangalia hicho kidonda kibichi na kumtangaza kuwa ni najisi kwa sababu huo ni ukoma.
16 Lakini hicho kidonda kikigeuka tena kuwa cheupe, mtu huyo atarudi kwa kuhani.
17 Kuhani atamwangalia na akiona kuwa kimegeuka kuwa cheupe, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi.
18 “Kama mtu ameshikwa na jipu, nalo limepona,
19 lakini mahali pale lilipokuwa jipu pamegeuka kuwa uvimbe mweupe au kuwa pekundu lakini peupe kiasi, ni lazima kumwonesha kuhani.
20 Kuhani atamwangalia huyo mtu. Kuhani akiona pamegeuka kuwa na shimo na nywele za mahali hapo zimegeuka kuwa nyeupe, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; huo ni ugonjwa wa ukoma ambao umetokana na jipu.
21 Lakini kama kuhani atamwangalia huyo mtu na kuona kuwa nywele za mahali hapo si nyeupe na wala hakuna shimo, ila pamefifia, basi, atamtenga huyo mtu kwa muda wa siku saba.
22 Kama ugonjwa huo utaenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; sehemu hiyo ina ugonjwa.
23 Lakini, kama ile sehemu haijaenea, basi, lile ni kovu la jipu tu. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi.
24 “Au, Iwapo kuna mahali palipoungua na ile nyama mbichi imegeuka kuwa nyekundu-nyeupe au ni nyeupe,
25 kuhani atapaangalia. Kama akiona kuwa nywele zimegeuka kuwa nyeupe na pana shimo, basi, huo ni ukoma. Ukoma huo umejitokeza kwa njia ya mahali hapo palipoungua. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; kwani anao ugonjwa wa ukoma.
26 Lakini kama kuhani akiona kuwa nywele za mahali hapo si nyeupe na hakuna shimo ila pamefifia, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda wa siku saba.
27 Siku ya saba kuhani atamwangalia. Kama umeenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; kwani anao ugonjwa wa ukoma.
28 Lakini, kama ile alama haijaenea, ila imefifia, huo ni uvimbe uliotokana na kuungua; basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi; kwani hilo ni kovu la kuungua.
29 “Kama mtu yeyote mwanamume au mwanamke, ana kidonda kichwani au kidevuni,
30 kuhani atauangalia ugonjwa huo. Iwapo kuhani ataona kuwa kuna shimo na nywele ni manjano na nyembamba, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; kwani huo ni upele na ni ukoma wa kichwa au wa kidevu.
31 Kama kuhani ataona kuwa hakuna shimo na nywele si nyeusi, basi kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda wa siku saba.
32 Siku ya saba kuhani atakiangalia kile kidonda. Kama kidonda hicho hakijaenea na hakuna nywele zenye rangi ya manjano wala hakuna vipele vyovyote mahali hapo, basi,
33 mtu huyo atanyoa nywele au ndevu zake. Lakini mahali pale penye vipele hatapanyoa. Kisha kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda mwingine wa siku saba.
34 Siku ya saba, kuhani ataviangalia vile vipele. Iwapo kuhani ataona kuwa vipele hivyo havikuenea kwenye ngozi na wala havikwenda ndani ya ngozi, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi. Mtu huyo atafua mavazi yake, naye atakuwa safi.
35 Lakini iwapo vipele hivyo vimeenea baada ya kutakaswa,
36 mtu huyo ataangaliwa na kuhani na ikiwa vimeenea kwenye ngozi, kuhani hatahitaji kutafuta nywele zenye rangi manjano; mtu huyo atakuwa najisi.
37 Lakini iwapo kuhani ataona kuwa vile vipele vimepona na nywele nyeusi zimeota mahali hapo, basi, vidonda hivyo vimepona, basi, mtu huyo ni safi. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi.
38 “Kama mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, ana alama nyeupe mwilini mwake,
39 kuhani atamwangalia mtu huyo. Iwapo kuhani ataona kuwa alama hizo ni nyeupe kiasi, huo ni upele wa kawaida; mtu huyo ni safi.
40 “Kama mwanamume amepata upara, yeye ni safi kwani ana upara tu.
41 Iwapo upara huo umetanda tangu nyuma mpaka mbele mtu huyo ana upara tu na yu safi.
42 Lakini kama kwenye kichwa penye upara au kwenye paji la uso penye upara kuna alama nyekundu-nyeupe, huo ni ukoma unaotokea kwenye upara wake kichwani au kwenye paji lake.
43 Kuhani atamwangalia. Iwapo kuhani ataona kuwa huo uvimbe ni mwekundu-mweupe kwenye upara au kwenye paji lake na unaonekana kama ukoma kwenye ngozi yake,
44 basi, mtu huyo ana ukoma; yeye ni najisi. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Ugonjwa wake upo kwenye kichwa chake.
45 “Mwenye ukoma yeyote atavaa nguo zilizochanika, nywele zake hatazichana, na mdomo wake wa juu ataufunika na atapaza sauti akisema, ‘Mimi ni najisi, mimi ni najisi.’
46 Ataendelea kuwa najisi kwa muda wote alio na ugonjwa huo. Yeye ni najisi; naye atakaa peke yake nje ya kambi.”
47 “Kama kuna namna ya upele wa ukoma kwenye vazi, liwe la sufu au kitani,
48 vazi hilo liwe limefumwa au limesokotwa kwa kitani au sufu au ni vazi la ngozi ya aina yoyote ile,
49 iwapo upele huo una rangi ya kijani au nyekundu katika vazi hilo, basi, vazi hilo lina upele. Kwa hiyo ni lazima kumwonesha kuhani.
50 Kuhani atauangalia upele huo na kuliweka vazi hilo kando kwa muda wa siku saba.
51 Siku ya saba atauangalia upele huo. Ikiwa upele huo umeenea katika vazi hilo, liwe ni la kufuma au kusokotwa au la ngozi au la ngozi ya aina yoyote ile, vazi hilo lina upele. Hivyo vazi hilo ni najisi.
52 Kuhani atalichoma moto vazi hilo kwani lina namna ya upele wa ukoma.
53 “Kama kuhani ataona kuwa upele haukuenea katika vazi, basi,
54 ataamuru vazi hilo lifuliwe na kuwekwa kando kwa muda mwingine wa siku saba.
55 Kuhani ataliangalia hilo vazi baada ya kuoshwa. Ikiwa ile alama haijabadilika rangi yake hata ingawa upele haukuenea, basi, vazi hilo ni najisi. Vazi hilo utalichoma moto, iwe alama ya upele ipo nyuma au mbele ya vazi hilo.
56 “Kama kuhani ataona kuwa ile alama imefifia baada ya kufuliwa, basi atararua ile sehemu iliyo na namna ya upele wa ukoma.
57 Kisha, ikiwa hiyo alama inaonekana tena baadaye katika vazi lililofumwa au lililosokotwa au katika kitu chochote cha ngozi, basi upele umeenea. Hapo vazi hilo utalichoma moto.
58 Lakini vazi ambalo upele umetokea baada ya kulifua itabidi lifuliwe mara ya pili na hivyo lipate kuwa safi.”
59 Hiyo ni sheria kuhusu namna ya upele wa ukoma unaotokea katika vazi la sufu au kitani au lililofumwa au lililosokotwa au la ngozi. Kwa njia hiyo mtaweza kupambanua kati ya vazi lisilo najisi na lile lililo najisi.