12 Basi Yeftha akatuma wajumbe waende kwa mfalme wa wana wa Amoni akasema, Je! Wewe una nini nami, hata umenijilia kupigana juu ya nchi yangu?
13 Mfalme wa wana wa Amoni akawajibu hao wajumbe wa Yeftha Kwa sababu Israeli waliitwaa nchi yangu, hapo walipokwea kutoka katika nchi ya Misri, tokea Arnoni mpaka Yaboki, na hata Yordani; basi sasa rudisha hizo nchi tena pasipo matata.
14 Yeftha akatuma wajumbe mara ya pili waende kwa huyo mfalme wa wana wa Amoni;
15 akamwambia, Yeftha akuambia hivi; Israeli hakuitwaa nchi ya Moabu, wala nchi ya wana wa Amoni;
16 lakini hapo walipokwea kutoka Misri, na Israeli walienenda katika bara hata kuifikilia Bahari ya Shamu, na kufikilia Kadeshi;
17 ndipo Israeli wakatuma wajumbe waende kwa mfalme wa Edomu, wakisema, Nakuomba sana unipe ruhusa nipite katika nchi yako; lakini mfalme wa Edomu hakusikia. Ni vivyo wakampelekea wajumbe mfalme wa Moabu; wala yeye hakukubali; basi Israeli wakakaa katika Kadeshi.
18 Kisha akaenda nyikani na kuizunguka hiyo nchi ya Edomu, na nchi ya Moabu, nao wakapita upande wa mashariki wa nchi ya Moabu, wakapanga marago upande wa pili wa Arnoni; wala hawakuingia ndani ya mpaka wa Moabu, kwa maana Arnoni ilikuwa ni mpaka wa Moabu.