1 Lakini sikia sasa, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na Israeli, niliyekuchagua;
2 BWANA, aliyekufanya, na kukuumba toka tumboni, yeye atakayekusaidia, asema hivi; Usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na wewe, Yeshuruni, niliyekuchagua.
3 Kwa maana nitamimina maji juu yake aliye na kiu, na vijito vya maji juu ya mahali pakavu; nitamwaga roho yangu juu ya wazao wako, na baraka yangu juu yao utakaowazaa;
4 nao watatokea katika manyasi, kama mierebi karibu na mifereji ya maji.
5 Mmoja atasema, Mimi ni wa BWANA; na mwingine atajiita kwa jina la Yakobo; na mwingine ataandika juu ya mkono wake, Kwa BWANA, na kujiita kwa jina la Israeli.
6 BWANA, Mfalme wa Israeli, Mkombozi wako, BWANA wa majeshi, asema hivi; Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu mimi hapana Mungu.
7 Naye ni nani kama mimi atakayeita, na kuyahubiri haya, na kunitengenezea, tangu nilipowaweka watu wa kale? Na mambo yanayokuja na yatakayotokea, wayatangaze.