1 Na mtu awaye yote akifanya dhambi, kwa kuwa ameisikia sauti yenye kuapisha, naye akawa ni shahidi, kwamba aliona au kujua, asipolifunua neno lile, ndipo atakapochukua uovu wake mwenyewe;
2 au kama mtu akigusa kitu kilicho najisi, kama ni mzoga wa mnyama wa nyikani aliye najisi, au kama ni mzoga wa mnyama wa mfugo aliye najisi, au kama ni mzoga wa mdudu aliye najisi, naye jambo hilo linamfichamania, akapata kuwa najisi, ndipo atakapochukua uovu wake;
3 au kama akiugusa uchafu wa binadamu, uchafu uwao wote ambao kwa huo amepata unajisi, na jambo hilo linamfichamania, hapo apatapo kulijua, ndipo atakapokuwa na hatia;
4 au, kama mtu akijiapisha, kwa kutamka haraka kwa midomo yake, kutenda uovu, au kutenda mema, neno lo lote mtu atakalolitamka kwa kiapo pasipo kufikiri, na neno hilo likamfichamania; hapo atakapolijua, ndipo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo;
5 kisha itakuwa, hapo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo, ndipo atakapoliungama jambo hilo alilolikosa;
6 naye atamletea BWANA sadaka yake ya hatia kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, mwana-kondoo wa kike, au mbuzi mke, kutoka katika kundi lake, kuwa ni sadaka ya dhambi; kisha kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake.
7 Lakini asipomweza mwana-kondoo, ndipo atakapomletea BWANA hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kuwa ni sadaka yake ya hatia ya jambo hilo alilolikosa; mmoja wa hao ndege kwa sadaka ya dhambi, na wa pili kwa sadaka ya kuteketezwa.