9 Naye Nehemia, ndiye aliyekuwa Tirshatha, na Ezra kuhani, mwandishi, na Walawi waliowafundisha watu, wakawaambia watu wote, Siku hii ni takatifu kwa BWANA, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati.
10 Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa BWANA wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya BWANA ni nguvu zenu.
11 Hivyo Walawi wakawatuliza watu wote, wakasema, Nyamazeni, kwa maana siku hii ni takatifu; wala msihuzunike.
12 Na watu wote wakaenda zao kula na kunywa, na kuwapelekea watu sehemu, na kufanya furaha nyingi, kwa sababu walikuwa wameyafahamu maneno yale waliyohubiriwa.
13 Hata siku ya pili wakuu wa mbari za mababa za watu wote, na makuhani, na Walawi, wakamkusanyikia Ezra, mwandishi, ili wapate kuyasikiliza maneno ya torati.
14 Wakaona ya kuwa imeandikwa katika torati, jinsi BWANA alivyoamuru kwa mkono wa Musa, ya kwamba wana wa Israeli wakae katika vibanda, katika sikukuu ya mwezi wa saba;
15 na ya kwamba wahubiri na kutangaza katika miji yao yote, na katika Yerusalemu, kusema, Enendeni mlimani, mkalete matawi ya mzeituni, na matawi ya mzeituni-mwitu, na matawi ya mihadasi, na matawi ya mitende, na matawi ya miti minene, ili kufanya vibanda, kama ilivyoandikwa.