2 Yasikieni maneno ya maagano haya; ukaseme na watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu;
3 ukawaambie, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Na alaaniwe mtu asiyeyasikia maneno ya maagano haya,
4 niliyowaamuru baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, katika tanuru ya chuma, nikisema, Itiini sauti yangu, mkafanye sawasawa na yote niwaagizayo ninyi; ndivyo mtakavyokuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu;
5 ili nipate kukitimiza kiapo nilichowaapia baba zenu, kuwapa nchi ijaayo maziwa na asali, kama ilivyo leo hivi. Ndipo nikajibu, nikasema, Amina, Ee BWANA.
6 Naye BWANA akaniambia, Hubiri maneno haya yote katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, ukisema, Yasikieni maneno ya maagano haya, mkayafanye.
7 Kwa maana naliwashuhudia sana baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, hata leo, nikiamka mapema na kuwashuhudia, nikisema, Itiini sauti yangu.
8 Lakini hawakutii, wala kutega masikio yao, bali walikwenda kila mtu katika ushupavu wa moyo wake mbaya; kwa hiyo nimeleta juu yao maneno yote ya maagano haya, niliyowaamuru wayafanye; lakini hawakuyafanya.