14 Kwa hiyo ningependelea wajane vijana waolewe, wapate watoto na kutunza nyumba zao ili maadui zetu wasipewe nafasi ya kusema mambo maovu juu yetu.
15 Kwa maana wajane wengine wamekwisha potoka na kumfuata Shetani.
16 Lakini kama mama Mkristo anao wajane katika jamaa yake, yeye anapaswa kuwatunza na si kuliachia kanisa mzigo huo, ili kanisa liweze kuwatunza wajane wale waliobaki peke yao kabisa.
17 Viongozi wa kanisa wanaowaongoza watu vizuri wanastahili kupata riziki maradufu, hasa wale wanaofanya bidii katika kuhubiri na kufundisha.
18 Maana Maandiko Matakatifu yasema: “Usimfunge ng'ombe kinywa anapopura nafaka,” na tena “Mfanyakazi astahili malipo yake.”
19 Usikubali kupokea mashtaka dhidi ya mzee yasipowakilishwa na mashahidi wawili au watatu.
20 Wale wanaotenda dhambi waonye hadharani, ili wengine wapate kuogopa.