1 Palitokea manabii wa uongo kati ya watu, na vivyo hivyo waalimu wa uongo watatokea kati yenu. Watu hao wataingiza mafundisho maharibifu na kumkana Bwana aliyewakomboa, na kwa njia hiyo watasababisha ghafla maangamizi yao wenyewe.
2 Tena watu wengi watazifuata hizo njia zao mbaya, na kwa sababu yao wengine wataipuuza njia ya ukweli.
3 Kwa tamaa yao mbaya watajipatia faida kwa kuwaambieni hadithi za uongo. Lakini kwa muda mrefu sasa Hakimu wao yuko tayari, na Mwangamizi wao yuko macho!
4 Malaika walipotenda dhambi, Mungu hakuwahurumia, bali aliwatupa katika moto wa Jehanamu ambako wamefungwa wakingojea siku ile ya hukumu.
5 Mungu hakuihurumia dunia ya hapo kale, bali alileta gharika kuu juu ya nchi ile ya watu wasiomcha Mungu; lakini Noa ambaye alihubiri uadilifu, Mungu alimwokoa pamoja na watu wengine saba.
6 Mungu aliiadhibu miji ya Sodoma na Gomora, akaiteketeza kwa moto, akaifanya iwe mfano wa mambo yatakayowapata watu wasiomcha Mungu.
7 Alimwokoa Loti, mtu mwema, ambaye alisikitishwa sana na mwenendo mbaya wa watu hao waasi.