3 Ninamshukuru Mungu ambaye ninamtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya wazee wangu; namshukuru kila ninapokukumbuka katika sala zangu usiku na mchana.
4 Nakumbuka machozi yako na ninatamani sana kukuona, ili nijazwe furaha.
5 Naikumbuka imani yako ya kweli, imani aliyokuwa nayo nyanya yako Loisi, na pia mama yako Eunike. Nina hakika kwamba wewe pia unayo.
6 Ndio maana nakukumbusha ukiweke motomoto kile kipaji ulichopewa na Mungu wakati nilipokuwekea mikono yangu.
7 Kwa maana Roho tuliyepewa na Mungu si wa kutufanya tuwe waoga; sivyo, ila ni Roho wa kutujalia upendo na nidhamu.
8 Basi, usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usione haya kwa sababu yangu mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Lakini shiriki katika mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unayopewa na Mungu.
9 Yeye alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si kwa sababu ya mastahili ya matendo yetu, bali kwa sababu ya kusudi lake na neema yake. Alitujalia neema hiyo kwa ajili ya Kristo Yesu kabla ya wakati,