26 Alipompata, alimleta Antiokia. Nao wote wawili walikaa na ile jumuiya ya kanisa kwa mwaka wote mzima wakifundisha kundi kubwa la watu. Huko Antiokia, ndiko kwa mara ya kwanza, wafuasi waliitwa Wakristo.
27 Wakati huohuo, manabii kadhaa walikuja Antiokia kutoka Yerusalemu.
28 Basi, mmoja wao aitwaye Agabo alisimama, na kwa uwezo wa Roho akabashiri kwamba kutakuwa na njaa kubwa katika nchi yote. (Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio).
29 Wale wanafunzi waliamua kila mmoja kwa kadiri ya uwezo wake apeleke chochote ili kuwasaidia wale ndugu waliokuwa wanaishi Yudea.
30 Basi, wakafanya hivyo na kuwapa Barnaba na Saulo mchango huo wauwasilishe wao wenyewe kwa wazee wa kanisa.