11 Mbona hamwelewi ya kwamba sikuwa nikisema juu ya mikate? Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!”
12 Hapo wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia wajihadhari siyo na chachu ya mikate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
13 Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?”
14 Wakamjibu, “Wengine wanasema kuwa ni Yohane Mbatizaji, wengine Elia, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.”
15 Yesu akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?”
16 Simoni Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”
17 Yesu akasema, “Heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana hakuna binadamu yeyote aliyekufunulia jambo hili, ila Baba yangu aliye mbinguni.