15 Yesu akawauliza, “Na nyinyi je, mnasema mimi ni nani?”
16 Simoni Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.”
17 Yesu akasema, “Heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana hakuna binadamu yeyote aliyekufunulia jambo hili, ila Baba yangu aliye mbinguni.
18 Nami nakuambia: Wewe ni Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala nguvu za kifo hazitaweza kulishinda.
19 Nitakupa funguo za ufalme wa mbinguni; kila utakachofunga duniani, kitafungwa pia mbinguni; kila utakachofungua duniani, kitafunguliwa pia mbinguni.”
20 Kisha akawaonya wanafunzi wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo.
21 Tangu wakati huo Yesu alianza kuwajulisha waziwazi wanafunzi wake kwamba ni lazima aende Yerusalemu, na huko kupata mateso mengi yatakayosababishwa na wazee, makuhani wakuu na waalimu wa sheria. Kwamba, atauawa na siku ya tatu atafufuliwa.