13 Kisha Yesu akasema, “Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa.
14 “Wakati huo itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ngambo: Aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake.
15 Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: Mmoja fedha talanta tano, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri.
16 Mara yule aliyekabidhiwa fedha talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano.
17 Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili.
18 Lakini yule aliyekabidhiwa fedha talanta moja akaenda, akachimba shimo ardhini, akaificha fedha ya bwana wake.
19 “Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya matumizi na mapato ya fedha yake.