2 Waambie wanaume wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu.
3 Hali kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe wachongezi au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema,
4 ili wawazoezeshe kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto,
5 wawe na kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa.
6 Kadhalika, wahimize vijana wawe na kiasi.
7 Katika mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe na uzito katika mafundisho yako.
8 Maneno yako yasiwe na hitilafu yoyote ili maadui zako waaibike wasipopata chochote kibaya cha kusema juu yetu.