4 Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa namna itakayodhihirisha siri hiyo.
5 Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini, mkitumia vizuri wakati mlio nao.
6 Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na yaliyokolezwa kwa chumvi na ya kuvutia, na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja.
7 Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote.
8 Ndiyo maana ninamtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa kuwaambieni habari zetu.
9 Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote yanayofanyika hapa.
10 Aristarko, ambaye yuko kifungoni pamoja nami, anawasalimuni; hali kadhalika Marko, binamu yake Barnaba, (mmekwisha pata maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni).