1 Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka katika serikali; maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu.
2 Anayepinga mamlaka ya viongozi anapinga agizo la Mungu; nao wafanyao hivyo wanajiletea hukumu wenyewe.
3 Maana, watawala hawasababishi hofu kwa watu wema, ila kwa watu wabaya. Basi, wataka usimwogope mtu mwenye mamlaka? Fanya mema naye atakusifu;
4 maana yeye ni mtumishi wa Mungu anayefanya kazi kwa faida yako. Lakini ukifanya mabaya, basi, huna budi kumwogopa, maana anao kweli uwezo wa kuadhibu. Yeye ni mtumishi wa Mungu, kuwaonesha ghadhabu yake wale watendao maovu.
5 Kwa hiyo ni lazima kuwatii wenye mamlaka, si tu kwa sababu ya kuogopa ghadhabu ya Mungu, bali pia kwa sababu dhamiri inadai hivyo.
6 Kwa sababu hiyohiyo nyinyi hulipa kodi; maana viongozi hao humtumikia Mungu ikiwa wanatimiza wajibu wao.