7 Mpeni kila mtu haki yake; mtu wa ushuru, ushuru; wa kodi, kodi; na astahiliye heshima, heshima.
8 Msiwe na deni kwa mtu yeyote, isipokuwa tu deni la kupendana. Ampendaye jirani yake ameitekeleza sheria.
9 Maana, amri hizi: “Usizini; Usiue; Usitamani;” na nyingine zote, zimo katika amri hii moja: “Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.”
10 Ampendaye jirani yake hamtendei vibaya. Basi, upendo ni utimilifu wa sheria.
11 Zaidi ya hayo, nyinyi mnajua tumo katika wakati gani: Sasa ndio wakati wa kuamka usingizini; naam, wokovu wetu uko karibu zaidi sasa kuliko wakati ule tulipoanza kuamini.
12 Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Basi, tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga.
13 Na tuishi kwa adabu kama inavyostahili wakati wa mchana, na wala sio kwa ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugomvi na wivu.