21 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:“Watu wote ambao hawakuambiwa habari zake wataona;nao wale ambao hawajapata kusikia, wataelewa.”
22 Kwa sababu hiyo nilizuiwa mara nyingi kuja kwenu.
23 Lakini maadamu sasa nimemaliza kazi yangu pande hizi, na kwa kuwa kwa miaka mingi nimekuwa na nia kubwa ya kuja kwenu,
24 natumaini kufanya hivyo sasa. Ningependa kuwaoneni nikiwa safarini kwenda Spania na kupata msaada wenu kwa safari hiyo baada ya kufurahia kuwa kwa muda pamoja nanyi.
25 Lakini, kwa sasa nakwenda kuwahudumia watu wa Mungu kule Yerusalemu.
26 Maana makanisa ya Makedonia na Akaya yemeamua kutoa mchango wao kuwasaidia watu wa Mungu walio maskini huko Yerusalemu.
27 Wao wenyewe wameamua kufanya hivyo; lakini, kwa kweli, hilo ni jukumu lao kwa hao. Maana, ikiwa watu wa mataifa mengine wameshiriki baraka za kiroho za Wayahudi, wanapaswa nao pia kuwahudumia Wayahudi katika mahitaji yao ya kidunia.