1 Ndugu zangu, mkiwa mnamwamini Bwana Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwabague watu kamwe.
2 Tuseme mtu mmoja ambaye amevaa pete ya dhahabu na mavazi nadhifu anaingia katika mkutano wenu, na papo hapo akaingia mtu maskini aliyevaa mavazi machafu.
3 Ikiwa mtamstahi zaidi yule aliyevaa mavazi ya kuvutia na kumwambia: “Keti hapa mahali pazuri,” na kumwambia yule maskini: “Wewe, simama huko,” au “Keti hapa sakafuni miguuni pangu,”
4 je, huo si ubaguzi kati yenu? Je, na huo uamuzi wenu haujatokana na fikira mbaya?
5 Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni! Mungu amechagua watu ambao ni maskini katika ulimwengu huu ili wapate kuwa matajiri katika imani na kupokea ufalme aliowaahidia wale wanaompenda.
6 Lakini nyinyi mnawadharau watu maskini! Je, matajiri si ndio wanaowakandamiza na kuwapeleka mahakamani?
7 Je, si haohao wanaolitukana hilo jina lenu zuri mlilopewa?