1 Baada ya tukio hilo, Absalomu alijipatia gari, farasi na watu hamsini wa kumtangulia.
2 Absalomu alizoea kuamka asubuhi na mapema na kwenda kusimama kwenye njia inayoelekea kwenye lango la mji. Mtu yeyote aliyekuwa na madai ambayo alitaka kuyapeleka kwa mfalme ili kupata uamuzi wake, Absalomu humwita mtu huyo kando na kumwuliza, “Unatoka mji gani?” Kama mtu huyo akisema ametoka mji fulani wa kabila la Israeli,
3 Absalomu humwambia, “Madai yako ni ya haki kabisa. Lakini hakuna mtu yeyote aliyeteuliwa na mfalme kukusikiliza.”
4 Tena, Absalomu humwambia, “Laiti mimi ningekuwa mwamuzi wa Israeli! Kila mtu mwenye madai au shauri angekuja kwangu, nami ningempa haki yake!”
5 Zaidi ya hayo, Absalomu alinyosha mkono wake akamkumbatia na kumbusu mtu yeyote aliyekuja kumwinamia na kumsujudu.
6 Basi, hivyo ndivyo Absalomu alivyowatendea Waisraeli wote waliokuja kutafuta uamuzi wa mfalme. Kwa kufanya hivyo, Absalomu aliiteka mioyo ya Waisraeli.
7 Baada ya miaka minne, Absalomu alimwambia mfalme, “Tafadhali uniruhusu niende huko Hebroni ili kutimiza nadhiri yangu ambayo nilimwekea Mwenyezi-Mungu;