30 Lakini Daudi aliendelea, akapanda Mlima wa Mizeituni huku analia, bila viatu na kichwa chake kimefunikwa. Hata watu wote waliokuwa pamoja naye walivifunika vichwa vyao wakawa wanapanda mlima huku wanalia.
31 Wakati huo, Daudi aliambiwa kuwa hata Ahithofeli alikuwa mmoja wa waasi waliojiunga na Absalomu. Lakini Daudi akaomba akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu nakuomba, uufanye mpango wa Ahithofeli usifanikiwe.”
32 Daudi alipofika kwenye kilele cha mlima, mahali pa kumwabudia Mungu, mtu mmoja jina lake Hushai kutoka Arki alikuja ili kumlaki, mavazi yake yakiwa yameraruka na kichwani pake kuna mavumbi.
33 Daudi akamwambia, “Ukienda pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu.
34 Lakini kama utarudi mjini Yerusalemu na kumwambia Absalomu, ‘Nitakuwa mtumishi wako, ee mfalme; kama vile nilivyokuwa mtumishi wa baba yako, hapo awali’; basi utanifanyia mpango wa Ahithofeli usifanikiwe.
35 Makuhani Sadoki na Abiathari wako pamoja nawe mjini! Basi, chochote utakachosikia kutoka nyumbani kwa mfalme, waambie makuhani Sadoki na Abiathari.
36 Tazama, watoto wao wawili wa kiume, Ahimaasi mwana wa Sadoki na Yonathani mwana wa Abiathari, wako pamoja nao. Na chochote mtakachosikia mtanipelekea habari kwa njia yao.”