1 Daudi alipokuwa amekipita kidogo kilele cha mlima, Siba mtumishi wa Mefiboshethi alimlaki Daudi akiwa na punda wawili ambao walikuwa wametandikwa huku wamebeba mikate200, vishada 100 vya zabibu kavu, matunda 100 ya kiangazi na kiriba cha divai.
2 Mfalme akamwuliza Siba, “Kwa nini umeleta vitu hivi?” Siba akamjibu, “Punda ni kwa ajili ya kupanda jamaa yako, mikate na matunda ya kiangazi ni kwa ajili ya vijana wote, nayo divai ni kwa ajili ya watakaozimia jangwani.”
3 Mfalme akamwuliza, “Mwana wa bwana wako yuko wapi?” Siba akamwambia mfalme, “Yeye amebaki mjini Yerusalemu kwa sababu anadhani kwamba watu wa Israeli watamrudishia ufalme wa Shauli babu yake.”
4 Mfalme akamwambia Siba, “Basi, yale yaliyokuwa mali ya Mefiboshethi sasa ni mali yako.” Siba akamwambia, “Nashukuru, bwana wangu mfalme, nami naomba nipate fadhili mbele yako daima.”
5 Wakati Daudi alipowasili kule Bahurimu, alitokea mtu mmoja wa ukoo wa Shauli, jina lake Shimei mwana wa Gera, akaanza kumlaani Daudi kwa mfululizo.
6 Akawa anamtupia mfalme Daudi mawe pamoja na watumishi wake. Watu wengine wote na mashujaa wakawa wanamzunguka Daudi upande wa kulia na kushoto.