17 Shimei alikwenda pamoja na Wabenyamini 1,000. Siba mtumishi wa jamaa ya Shauli, pamoja na watoto wake kumi na watumishi ishirini, walikwenda haraka mtoni Yordani kumtangulia mfalme Daudi.
18 Basi, wakavuka kwenye kivuko ili kuisindikiza jamaa ya mfalme na kumfanyia mfalme yote aliyoyapenda. Shimei mwana wa Gera akaja, akajitupa mbele ya mfalme, akasujudu, wakati mfalme alipokuwa karibu kuvuka mto Yordani.
19 Shimei akamwambia mfalme, “Nakuomba, bwana wangu mfalme, usinihesabu kuwa na hatia wala kukumbuka kosa nililofanya siku ile ulipokuwa ukiondoka mjini Yerusalemu. Nakuomba usiyaweke hayo maanani.
20 Maana, mimi mtumishi wako ninajua kwamba nilitenda dhambi. Hii ndiyo sababu nimekuja leo, nikiwa wa kwanza katika kabila la Yosefu, kuja kukulaki wewe bwana wangu, mfalme.”
21 Ndipo Abishai mwana wa Seruya akasema, “Je, si lazima Shimei auawe maana alimlaani mtu ambaye Mwenyezi-Mungu amemteua kwa kumpaka mafuta?”
22 Lakini Daudi akasema, “Wana wa Seruya, sina lolote nanyi; kwa nini mjifanye kama maadui zangu leo? Je, auawe mtu yeyote katika Israeli siku ya leo? Je, sijui kuwa mimi ni mfalme wa Israeli siku ya leo?”
23 Kisha, mfalme akamwambia Shimei, “Wewe hutauawa.” Mfalme akamwapia Shimei.