2 Kwa hiyo, ushindi wa siku hiyo uligeuzwa kuwa maombolezo kwa watu wote, waliposikia kuwa mfalme anamwombolezea Absalomu.
3 Hivyo, siku hiyo, watu waliingia mjini kimyakimya kama watu wanaorudi mjini wakiona aibu kwa kukimbia vita.
4 Mfalme alijifunika uso wake na kulia kwa sauti kubwa akisema, “Ole mwanangu Absalomu! Ole, Absalomu, mwanangu! Mwanangu!”
5 Ndipo Yoabu alipoingia nyumbani kwa mfalme, akamwambia, “Leo umetuaibisha sisi watumishi wako wote ambao leo tumeyaokoa maisha yako, maisha ya watoto wako wa kiume, na maisha ya watoto wako wa kike, maisha ya wake zako na maisha ya masuria wako.
6 Wewe unawapenda wale wanaokuchukia na unawachukia wale wanaokupenda. Umetuonesha waziwazi leo kwamba makamanda na watumishi wako hawana maana kwako. Naona kuwa leo, kama Absalomu angekuwa hai, na sisi sote tungalikuwa tumekufa, wewe ungefurahi.
7 Sasa, simama uzungumze na watumishi wako kwa upole. Maana, naapa kwa Mwenyezi-Mungu kwamba, kama huendi kuzungumza nao, hakuna hata mmoja atakayebaki pamoja nawe leo jioni. Hili litakuwa jambo baya zaidi kwako kuliko maovu yote yaliyokupata tangu ujana wako hadi leo.”
8 Kisha, mfalme akatoka akaenda, akaketi mahali pake karibu na lango. Watu wote walipoambiwa kuwa mfalme yuko langoni, wote walimwendea.Wakati huo, watu wote wa Israeli walikuwa wamekimbia, kila mmoja nyumbani kwake.