10 Kisha, Rispa binti Aya alichukua nguo ya gunia, akajitandikia mwambani. Alikaa hapo tangu mwanzo wa mavuno mpaka wakati wa mvua ulipowadia na kuinyeshea maiti. Wakati huo wote, aliwafukuza ndege wa angani na wanyama wa porini, usiku na mchana, ili wasifikie maiti hizo.
11 Daudi aliposikia yale aliyofanya Rispa binti Aya, suria wa Shauli,
12 alikwenda na kuichukua mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe kutoka wakazi wa Yabesh-gileadi, waliokuwa wameiiba kutoka mtaani huko Beth-sheani, ambako Wafilisti walikuwa wamemtundika Shauli na Yonathani siku ile Wafilisti walipomuua Shauli mlimani Gilboa.
13 Basi, Daudi akairudisha mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe kutoka huko; halafu wakakusanya mifupa ya vijana saba waliotundikwa.
14 Basi, watu wa Daudi wakaizika mifupa ya Shauli na Yonathani mwanawe katika nchi ya Benyamini, huko Sela katika kaburi la Kishi baba yake Shauli. Walifanya kila kitu ambacho mfalme aliamuru. Baada ya hayo, Mungu akayasikiliza maombi kuhusu nchi yao.
15 Kisha Wafilisti walifanya vita tena na Waisraeli. Naye Daudi na watu wake wakaenda kupigana na Wafilisti. Daudi alichoka sana siku hiyo.
16 Ishbi-benobu, mmojawapo wa wazawa wa majitu ambaye mkuki wake wa shaba ulikuwa na uzito wa karibu kilo tatu na nusu na aliyekuwa amejifunga upanga mpya alisema atamuua Daudi.