9 Maana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu.
10 Ninyi ni mashahidi, na Mungu pia, jinsi tulivyokaa kwenu ninyi mnaoamini, kwa utakatifu, na kwa haki, bila kulaumiwa;
11 vile vile, kama mjuavyo, jinsi tulivyomwonya kila mmoja wenu kama baba awaonyavyo watoto wake mwenyewe, tukiwatia moyo na kushuhudia;
12 ili mwenende kama ilivyo wajibu wenu kwa Mungu, mwenye kuwaita ninyi ili mwingie katika ufalme wake na utukufu wake.
13 Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.
14 Maana ninyi, ndugu, mlikuwa wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyo katika Uyahudi, katika Kristo Yesu; kwa kuwa mlipata mateso yale yale kwa watu wa taifa lenu wenyewe, waliyoyapata na hao kwa Wayahudi;
15 ambao walimwua Bwana Yesu, na hao manabii, na kutuudhi sisi; wala hawampendezi Mungu, wala hawapatani na watu wo wote;