1 Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote;
2 bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba.
3 Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia.
4 Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,
5 kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.
6 Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.