1 Maana nataka ninyi mjue jinsi ilivyo kuu juhudi yangu niliyo nayo kwa ajili yenu, na kwa ajili ya wale wa Laodikia, na wale wasioniona uso wangu katika mwili;
2 ili wafarijiwe mioyo yao, wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo;
3 ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika.
4 Nasema neno hili, mtu asije akawadanganya kwa maneno ya kuwashawishi.
5 Maana nijapokuwa sipo kwa mwili, lakini nipo pamoja nanyi kwa roho, nikifurahi na kuuona utaratibu wenu na uthabiti wa imani yenu katika Kristo.
6 Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye;
7 wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani.