1 Yeye aliye dhaifu wa imani, mkaribisheni, walakini msimhukumu mawazo yake.
2 Mtu mmoja anayo imani, anakula vyote; lakini yeye aliye dhaifu hula mboga.
3 Yeye alaye asimdharau huyo asiyekula, wala yeye asiyekula asimhukumu huyo alaye; kwa maana Mungu amemkubali.
4 Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha.
5 Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.
6 Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu.
7 Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake.