1 Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Enendeni, mkavimimine vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi.
2 Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake.
3 Na huyo wa pili akakimimina kitasa chake juu ya bahari, ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa.
4 Na huyo wa tatu akakimimina kitasa chake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu.
5 Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi;
6 kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili.
7 Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako.