2 Akalia kwa sauti kuu, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli ule mkuu; umekuwa maskani ya mashetani, na ngome ya kila roho mchafu, na ngome ya kila ndege mchafu mwenye kuchukiza;
3 kwa kuwa mataifa yote wamekunywa mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake, na wafalme wa nchi wamezini naye, na wafanya biashara wa nchi wamepata mali kwa nguvu za kiburi chake.
4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni, ikisema, Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake.
5 Kwa maana dhambi zake zimefika hata mbinguni, na Mungu amekumbuka maovu yake.
6 Mlipeni kama yeye alivyolipa, mkamlipe mara mbili kwa kadiri ya matendo yake. Katika kikombe kile alichokichanganyisha, mchanganyishieni maradufu.
7 Kwa kadiri alivyojitukuza na kufanya anasa, mpeni maumivu na huzuni kadiri iyo hiyo. Kwa kuwa husema moyoni mwake, Nimeketi malkia, wala si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.
8 Kwa sababu hiyo mapigo yake yatakuja katika siku moja, mauti, na huzuni, na njaa, naye atateketezwa kabisa kwa moto. Kwa maana Bwana Mungu aliyemhukumu ni mwenye nguvu.