8 Kwa maana wanafunzi wake wamekwenda mjini kununua chakula.
9 Basi yule mwanamke Msamaria akamwambia, Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria? (Maana Wayahudi hawachangamani na Wasamaria.)
10 Yesu akajibu, akamwambia, Kama ungaliijua karama ya Mungu, naye ni nani akuambiaye, Nipe maji ninywe, ungalimwomba yeye, naye angalikupa maji yaliyo hai.
11 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, huna kitu cha kutekea, na kisima ni kirefu; basi umeyapata wapi hayo maji yaliyo hai?
12 Je! Wewe u mkubwa kuliko baba yetu, Yakobo, aliyetupa kisima hiki, naye mwenyewe akanywa maji yake, na wanawe pia, na wanyama wake?
13 Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena;
14 walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.