1 Na baada ya hayo Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua.
2 Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa karibu.
3 Basi ndugu zake wakamwambia, Ondoka hapa, uende Uyahudi, wanafunzi wako nao wapate kuzitazama kazi zako unazozifanya.
4 Kwa maana hakuna mtu afanyaye neno kwa siri, naye mwenyewe ataka kujulikana. Ukifanya mambo haya, basi jidhihirishe kwa ulimwengu.
5 Maana hata nduguze hawakumwamini.
6 Basi Yesu akawaambia, Haujafika bado wakati wangu; ila wakati wenu sikuzote upo.
7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi; bali hunichukia mimi, kwa sababu mimi naushuhudia ya kuwa kazi zake ni mbovu.