59 Na maneno yangu haya, niliyoyaomba mbele za BWANA, na yawe karibu na BWANA, Mungu wetu, mchana na usiku, ili aitetee haki ya mtumishi wake, na haki ya watu wake Israeli, kwa kadiri ya haja zao za kila siku.
60 Watu wote wa ulimwengu wajue ya kuwa BWANA ndiye Mungu; hakuna mwingine.
61 Mioyo yenu na iwe kamili kwa BWANA, Mungu wetu, kuenenda katika sheria zake, na kuzishika amri zake, kama ilivyo leo.
62 Ndipo mfalme, na Israeli wote pamoja naye, wakatoa sadaka mbele za BWANA.
63 Sulemani akatoa sadaka za amani, alizomtolea BWANA, ng’ombe ishirini na mbili elfu, na kondoo mia na ishirini elfu. Ndivyo mfalme na wana wa Israeli wote walivyoifanya wakfu nyumba ya BWANA.
64 Siku ile ile mfalme akaitakasa behewa ya katikati iliyokuwa mbele ya nyumba ya BWANA; kwa kuwa hapo ndipo alipotoa sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na mafuta ya sadaka za amani; kwa sababu ile madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za BWANA ilikuwa ndogo, haikutosha kuzipokea sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na mafuta ya sadaka za amani.
65 Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, kutoka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, mbele za BWANA, Mungu wetu, siku saba na siku saba, yaani siku kumi na nne.