3 Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako.
4 Samweli akafanya hayo aliyosema BWANA, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani?
5 Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea BWANA dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu.
6 Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake.
7 Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo.
8 Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, BWANA hakumchagua huyu.
9 Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, wala BWANA hakumchagua huyu.