10 Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake.
11 Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili.
12 Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli.
13 Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu.
14 Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye BWANA alikuwa pamoja naye.
15 Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa.
16 Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao.