11 Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili.
12 Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli.
13 Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu.
14 Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye BWANA alikuwa pamoja naye.
15 Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa.
16 Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao.
17 Kisha Sauli akamwambia Daudi, Tazama, binti yangu mkubwa, Merabu, huyu nitakupa wewe ili umwoe; ila na wewe uniwie hodari wa vita, na kuvipiga vita vya BWANA. Maana Sauli alisema moyoni mwake, Mkono wangu usiwe juu yake, bali mkono wa Wafilisti na uwe juu yake.