33 Sauli akamtupia mkuki wake ili kumpiga; basi Yonathani akajua ya kuwa baba yake ameazimu kumwua Daudi.
34 Basi Yonathani akaondoka pale mezani, mwenye hasira kali, wala hakula chakula siku ya pili ya mwezi, kwa sababu alimhuzunikia Daudi sana, na kwa sababu baba yake amemwaibisha.
35 Hata asubuhi Yonathani akatoka kwenda shambani wakati ule alioagana na Daudi, na mtoto mdogo alikuwa pamoja naye.
36 Akamwambia mtoto wake, Piga mbio, ukaitafute mishale niipigayo. Na yule mtoto alipokuwa akipiga mbio, akapiga mshale, ukapita juu yake.
37 Na mtoto alipofika penye ule mshale alioupiga Yonathani, Yonathani akampigia mtoto kelele, akasema, Je! Mshale si huko mbele yako?
38 Yonathani akampigia mtoto kelele, Haya! Hima! Usikawie. Mtoto wa Yonathani akaikusanya mishale, akaenda kwa bwana wake.
39 Lakini yule mtoto hakujua lo lote. Yonathani na Daudi ndio walioijua habari yenyewe.