3 Naye Sauli akapiga hema katika kilima cha Hakila, kilichoelekea Yeshimoni, barabarani; lakini Daudi alikuwa akikaa nyikani, akaona ya kwamba Sauli amemfuata mpaka nyikani.
4 Basi Daudi akatuma wapelelezi, akapata habari ya hakika ya kwamba Sauli amefika.
5 Daudi akainuka, akafika mahali pale alipotua Sauli; Daudi akapaangalia mahali alipolala Sauli, na Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi lake; naye Sauli alikuwa amelala kati ya magari, na hao watu wamepiga hema zao wakimzunguka.
6 Ndipo Daudi akajibu, akamwambia Ahimeleki, Mhiti, na Abishai, mwana wa Seruya, ndugu yake Yoabu, akisema, Ni nani atakayeshuka pamoja nami kwa Sauli kambini? Abishai akasema, Mimi nitashuka pamoja nawe.
7 Basi Daudi na Abishai wakawaendea watu usiku; na tazama, Sauli alikuwapo kati ya magari amelala usingizi, na fumo lake limechomekwa chini, karibu na kichwa chake; naye Abneri na watu wake wamelala wakimzunguka.
8 Ndipo Abishai akamwambia Daudi, Mungu amemtia adui yako mikononi mwako leo; basi, niache nimpige kwa hilo fumo hata nchi kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili.
9 Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi wa BWANA, naye akawa hana hatia?