1 Ndipo Daudi aliposema moyoni mwake, Siku moja, basi, mimi nitaangamia kwa mkono wa Sauli; hakuna jema zaidi kwangu kuliko kukimbia mpaka nchi ya Wafilisti; naye Sauli atakata tamaa kwa habari yangu, asinitafute tena mipakani mwote mwa Israeli; hivyo nitaokoka katika mikono yake.
2 Basi Daudi akaondoka, yeye na hao watu mia sita aliokuwa nao, akamvukia Akishi, mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi.
3 Daudi akakaa huko Gathi pamoja na Akishi, yeye na watu wake, kila mtu na watu wa nyumbani mwake; Daudi naye alikuwa na wakeze wawili, Ahinoamu wa Yezreeli, na Abigaili wa Karmeli, aliyekuwa mkewe Nabali.
4 Naye Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia mpaka Gathi; wala hakumtafuta tena.
5 Daudi akamwambia Akishi, Sasa kama nimeona kibali machoni pako na nipewe mahali katika miji hii mmojawapo mashambani, nipate kukaa huko; mbona mtumwa wako akae katika mji wa kifalme pamoja na wewe?
6 Ndipo Akishi akampa Siklagi siku ile; kwa sababu hiyo huo mji wa Siklagi ni mali ya wafalme wa Yuda hata hivi leo.