1 Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote,
2 mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.
3 Nathani akamwambia mfalme, Haya, fanya yote yaliyomo moyoni mwako; maana BWANA yu pamoja nawe.
4 Ikawa usiku uo huo, neno la BWANA likamfikia Nathani kusema,
5 Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, BWANA asema hivi, Je! Wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake?
6 Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani.
7 Mahali mwote nilimokwenda na wana wa Israeli wote, je! Nimesema neno lo lote na mtu ye yote wa waamuzi wa Israeli, niliyemwagiza kuwalisha watu wangu Israeli, nikisema, Mbona hamkunijengea nyumba ya mierezi?