1 Katika mwaka wa tatu wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alikwenda Yerusalemu akauhusuru.
2 Bwana akamtia Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika mkono wake, pamoja na baadhi ya vyombo vya nyumba ya Mungu; naye akavichukua mpaka nchi ya Shinari, mpaka nyumba ya mungu wake; akaviingiza vile vyombo katika nyumba ya hazina ya mungu wake.
3 Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana;
4 vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao.
5 Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme.
6 Basi katika hao walikuwapo baadhi ya wana wa Yuda, Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria.