13 Ndipo Danieli akaletwa mbele ya mfalme. Na Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Je! Wewe ndiwe Danieli yule, aliye mmoja wa wana wa Yuda waliohamishwa, ambao mfalme, baba yangu, aliwaleta huku toka Yerusalemu?
14 Nimesikia habari zako, kwamba roho ya miungu imo ndani yako, na kwamba nuru na ufahamu na akili bora zimeonekana kwako.
15 Basi sasa, watu wenye hekima na wachawi wameletwa mbele yangu, wapate kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake; lakini hawakuweza kunijulisha tafsiri ya jambo hili.
16 Lakini nimesikia habari zako, kwamba waweza kuleta tafsiri, na kufumbua mafumbo; haya! Kama ukiweza kulisoma andiko hili, na kunijulisha tafsiri yake, utavikwa mavazi ya rangi ya zambarau, na kuwa na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utakuwa mtu wa tatu katika ufalme.
17 Ndipo Danieli akajibu, akasema mbele ya mfalme; Zawadi zako zishike wewe mwenyewe; na thawabu zako mpe mtu mwingine; walakini nitamsomea mfalme maandiko haya, na kumjulisha tafsiri yake.
18 Kwa habari zako, Ee mfalme, Mungu Aliye juu alimpa Nebukadreza, baba yako, ufalme, na ukuu, na fahari, na utukufu;
19 na kwa sababu ya ule ukuu aliompa, watu wa kabila zote, na mataifa, na lugha, wakatetemeka na kuogopa mbele yake; aliyetaka kumwua alimwua; na aliyetaka kumwacha hai, alimwacha hai; aliyetaka kumtukuza, alimtukuza; na aliyetaka kumshusha, alimshusha.