17 Basi sasa, Ee Mungu wetu, yasikilize maombi ya mtumishi wako, na dua zake, ukaangazishe uso wako juu ya patakatifu pako palipo ukiwa, kwa ajili ya Bwana.
18 Ee Mungu wangu, tega sikio lako, ukasikie; fumbua macho yako ukautazame ukiwa wetu, na mji ule ulioitwa kwa jina lako; maana hatukutolei maombi yetu kwa sababu ya haki yetu, lakini kwa sababu ya rehema zako nyingi.
19 Ee Bwana, usikie; Ee Bwana, usamehe; Ee Bwana, usikilize, ukatende, usikawie; kwa ajili yako wewe, Ee Mungu wangu; kwa sababu mji wako na watu wako wanaitwa kwa jina lako.
20 Basi hapo nilipokuwa nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu Israeli, na kuomba dua yangu mbele za BWANA, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu;
21 naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni.
22 Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danieli, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu.
23 Mwanzo wa maombi yako ilitolewa amri, nami nimekuja kukupasha habari; maana wewe unapendwa sana; basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya.