5 Basi palikuwa na Myahudi mmoja huko Shushani ngomeni; jina lake Mordekai, bin Yairi, bin Shimei, bin Kishi, wa kabila ya Benyamini;
6 ambaye kwamba amechukuliwa mateka kutoka Yerusalemu miongoni mwa wafungwa waliochukuliwa pamoja na Yekonia, mfalme wa Yuda; ambaye Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alimchukua.
7 Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo mzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake yeye.
8 Basi ikawa, wakati iliposikiwa amri ya mfalme na mbiu yake, wasichana wengi wakakusanyika huko Shushani ngomeni mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake.
9 Yule mwanamwali akampendeza, akapokea fadhili kwake; naye akampa upesi vifaa vya utakaso, pamoja na posho zake, na vijakazi saba walio haki yake, wa nyumbani mwa mfalme. Pia akamhamisha yeye na vijakazi wake akawaweka mahali pazuri katika nyumba ya wanawake.
10 Walakini Esta hakudhihirisha kabila yake wala jamaa yake, kwa maana ndivyo alivyomwagiza Mordekai asiwadhihirishe.
11 Na yule Mordekai akawa akitembea kila siku mbele ya ua wa nyumba ya wanawake, ili ajue hali yake Esta, na hayo yatakayompata.